Jumatano, 25 Mei 2016

Tanzania ya viwanda yaanza kuonyesha sura yake

NDOTO ya Tanzania kuwa nchi ya
viwanda, inaelekea kutimia baada ya
Serikali ya Awamu ya Tano kuonesha
kwa vitendo dhamira yake ya
kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.
Tangu wakati wa kampeni Ilani ya CCM
ya mwaka 2015 iliponadiwa pamoja na
kauli mbalimbali za wagombea wa
chama hicho wakiongozwa na aliyekuwa
mgombea urais, Dk John Magufuli, ahadi
kubwa ilikuwa ni kujenga uchumi wa nchi
kupitia viwanda. Ahadi hiyo inatokana na
ukweli kuwa Tanzania imedhamiria
kuhakikisha ifikapo mwaka 2025,
inakuwa ni miongoni mwa nchi zilizo na
uchumi wa kati.
Katika kuhakikisha ndoto hiyo inatimia,
kupitia bajeti ya kwanza chini ya Serikali
ya Awamu ya Tano ya Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
kipaumbele kikubwa kimewekwa katika
sekta nzima ya viwanda. Hali hiyo
ilijidhihirisha tangu, Serikali ilipowasilisha
mapendekezo ya kiwango cha ukomo wa
bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha
2016/17 ambayo inaonesha kuwa
itatumika Sh trilioni 29.53 ikiwa ni
ongezeko la trilioni 7 ikilinganishwa na
bajeti ya mwaka wa fedha uliopita.
Sura hiyo ya bajeti ya mwaka 2016/17
inatofautiana na iliyopita iliyokuwa ya Sh
trilioni 22.45 katika maeneo mengi, ikiwa
ni pamoja na kiwango cha fedha
kitakachotengwa kwa ajili ya shughuli za
maendeleo, ambacho ni zaidi ya mara
mbili ya fedha za eneo hilo katika bajeti
iliyopita. Aidha katika mapendekezo hayo
yaliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk
Philip Mpango, shughuli zitakazopewa
kipaumbele kwenye mipango hiyo ya
maendeleo zimegawanywa katika
maeneo manne.
Maeneo hayo ni viwanda vya kukuza
uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi
wa viwanda, kufungamanisha maendeleo
ya uchumi na rasilimali watu, mazingira
wezeshi kwa uendeshaji biashara na
uwekezaji na pia usimamizi wa
utekelezaji wa mpango. Katika
kuthibitisha azma hiyo kwa vitendo,
Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Charles Mwijage,
anapowasilisha hivi karibuni bungeni
Dodoma makadirio ya mapato na
matumizi kwa mwaka wa fedha wa
2016/17 ya wizara hiyo, alibainisha wazi
kuwa kipaumbele kikubwa katika bajeti
hiyo ni kuinua sekta ya viwanda.
Anasema katika kutimiza dhana ya
Serikali ya kuijenga Tanzania yenye
uchumi wa viwanda, wizara yake
imejipanga kuhamasisha sekta binafsi
miongoni mwa Watanzania na wageni
kuwekeza kwenye sekta ya viwanda
vidogo, vya kati na vikubwa. Anasema
Serikali itawekeza nguvu zaidi kwenye
viwanda vidogo na vya kati (SMEs) kwa
kuwa ndio kwa sasa vinavyoongoza
nchini kwa kutengeneza ajira na
kuongeza pato la mtu mmoja mmoja.
Anafafanua kuwa kwa mujibu wa utafiti
uliofanywa na wizara hiyo, sekta ya
SMEs imetengeneza ajira takribani milioni
52 za Watanzania na kuchangia asilimia
28 kwenye Pato la Taifa (GDP). “Wizara
hii itawezesha upatikanaji wa maeneo ya
kujenga viwanda na kutoa ushauri
kuhusu upatikanaji wa mitaji na teknolojia
za kisasa. “Kwa ujumla wizara itabeba
jukumu la kuibua wana viwanda,
kuwakuza na kuwaendeleza,” anasisitiza
Mwijage.
Anaeleza kuwa kwa kuzingatia msimamo
huo, wizara hiyo itahakikisha viwanda
vilivyopo vinafanya kazi kwa uwezo
mkubwa kadri iwezekanavyo ili kudhibiti
bidhaa za nje zinazoingia nchini bila
ushindani ulio sawa. Anasema pia wizara
hiyo itaondoa vikwazo vinavyopunguza
uwezo wa kiushindani kwa viwanda
vilivyopo nchini, itahamasisha wananchi
kuwekeza katika sekta ya viwanda na
itahamasisha wawekezaji wakubwa wa
ndani na nje ya nchi kuwekeza katika
sekta hiyo.
“Nawaahidi, tutapigana kufa au kupona ili
tuwe na miundombinu wezeshi na saidizi
iliyo tayari katika maeneo ya uwekezaji
ngazi ya kanda na taifa. Nawashawishi
wazawa wanaomiliki viwanda huu ndio
wakati. Tutalinda viwanda vyenu , siwezi
kulisha mtoto wa kware, na kuacha
mtoto wa kuku afe,” anasema.
Akizungumzia maendeleo ya viwanda
nchini, Mwijage anabainisha kuwa idadi
ya viwanda nchini imeendelea
kuongezeka kutoka viwanda 125 mwaka
1961 baada ya Tanzania kupata Uhuru
hadi kufikia viwanda 49,243 mwaka
2013.
Anasema kutokana na ukweli huo
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga
kuhakikisha inatimiza kwa kutekeleza
ahadi yake ya kuijenga Tanzania ya
viwanda kwa kuhakikisha viwanda
vinajengwa na kusambazwa nchi nzima.
Kwa mujibu wa Serikali kasi ya ukuaji wa
viwanda imekua kati ya mwaka 2006
hadi mwaka 2013 ambapo vimeongezeka
kutoka viwanda 5,153 mwaka 2005 hadi
viwanda 49,243 mwaka 2013.
Pamoja na hayo, Mwijage anabainisha
kuwa ni lengo la Serikali ya Awamu ya
Tano kuona viwanda vyote
vilivyobinafsishwa vinafanyakazi ambapo
hadi sasa ni kati ya viwanda 106
vilivyofanyiwa tathmini, 45 vinafanya kazi
vizuri, 24 vinasuasua na 37 vimefungwa.
Anasema kutokana na ongezeko hilo la
viwanda, viwanda vikubwa vinavyoajiri
kuanzia watu 100 ni 247, viwanda vya
kati vinavyoajiri kati ya watu 50 na 99 ni
170, viwanda vidogo vinavyoajiri kati ya
watu watano na 49 ni 6,907 na viwanda
vidogo sana vinavyoajiri chini ya watu
watano ni 41,919.
Anasisitiza kuwa ni lengo la Serikali ya
Awamu ya Tano kuona kuwa viwanda
vyote vilivyobinafsishwa vinafanya kazi.
“Viongozi wakuu wa nchi wamekuwa
wakisisitiza utekelezaji wa lengo hilo na
wizara yetu kwa kushirikiana na Msajili
wa Hazina tunafuatilia jukumu hilo siku
hadi siku,” anasema. Anafafanua kuwa
mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa
viwanda 37 vilivyofungwa baada ya
kubinafsishwa vinafanyiwa tathmini
haraka kabla ya nusu ya kwanza ya
mwaka wa fedha unaoanza Julai Mosi,
mwaka huu.
“Nasisitiza kabisa kuhusu kuwa hatma
ya viwanda visivyofanya kazi ni kwa
wamiliki waliopewa kutekeleza mikataba
ya mauzo au kupewa wawekezaji wapya
ili waviendeshe,” anasema. Aidha,
Mwijage anaeleza kuwa kupitia bajeti
hiyo na mikakati ambayo Serikali hiyo
imejiwekea, itahakikisha inahimiza na
kusimamia mpango wa viwanda sehemu
zote za nchi. Anasema tayari mamlaka
za mikoa na wilaya zimeelekezwa
kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli ya
viwanda na biashara.
“Hapa tutahakikisha kila eneo linakuwa
na kiwanda kulingana na mahitaji ya eneo
husika. Kwa mfano Tanga wanalima sana
matunda hivyo viwanda vyake vitajikita
katika eneo la kuzalisha bidhaa za
matunda kama vile juisi.” Mwijage
alisema katika kutimiza dhana ya kujenga
Tanzania yenye uchumi wa viwanda,
Wizara ya Viwanda imejipanga
kuhamasisha sekta binafsi kwa
Watanzania na wageni kuwekeza kwenye
sekta ya viwanda vidogo, vya kati na
vikubwa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Viwanda na Biashara, Vicky
Kamata anapongeza hatua ya Serikali ya
Awamu ya Tano ya kuleta mapinduzi ya
viwanda na kushauri hatua madhubuti
zichukuliwe katika kushughulikia
changamoto zinazoweza kukwamisha
ndoto hiyo. “Serikali iweke kipaumbele
katika suala la kutenga ardhi kwa ajili ya
viwanda kwa kushirikisha halmashauri
za wilaya na mikoa ikiwa ni pamoja na
kujenga miundombinu bora kama vile
barabara, reli, maji, umeme na
mawasiliano,” anasisitiza

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni