MEIMOSI
Mhe. Samia Hassan, Makamu wa Rais;
Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu;
Ndugu Gratian Mukoba, Rais wa Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA);
Mama Nortubunga Maskini, Makamu wa Rais wa
TUCTA;
Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu;
Mhe. Tulia Ackson, Naibu Spika;
Balozi Injinia John Kijazi, Katibu Mkuu Kiongozi;
Mheshimiwa Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma;
Waheshimiwa Mawaziri wote, na Waheshimiwa
Wabunge mliopo;
Bi. Mary Kawar, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi
Duniani (ILO), Ofisi ya Nchi za Afrika Mashariki;
Waheshimiwa Mabalozi mliopo;
Waheshimiwa Majaji,
Mheshimiwa Almas Maige, Mwenyekiti wa Chama
cha Waajiri Tanzania;
Dr. Aggrey Mlimuka, Mkurugenzi Mtendaji wa
Chama cha Waajiri Tanzania (ATE);
Ndugu Nicholaus Mgaya, Katibu Mkuu wa Shirikisho
la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA);
Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi;
Viongozi na Maafisa wa Serikali mliopo;
Wawakilishi wa Vyama vya Siasa mliopo; Mzee
Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
Bwana Kimbisa (Mb), Mwenyekiti wa CCM Mkoa;
Wanahabari;
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma;
Ndugu Wananchi;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutupa uhai na afya njema na kuweza
kukutana hapa. Leo ni siku muhimu sana. Tupo
hapa kwa ajili ya kuenzi na kuthamini mchango wa
wafanyakazi wa Tanzania, wake kwa waume,
walioko sekta binafsi na ya umma, na ambao kila
siku tangu asubuhi hadi jioni wamekuwa wakivuja
jasho kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu.
Hii si mara yangu ya kwanza nashiriki Sherehe ya
Siku ya Wafanyakazi, maarufu kama Mei Mosi.
Nimeshiriki kwenye sherehe hizi mara kadhaa.
Lakini leo nashiriki kipekee kabisa. Nashiriki kwa
mara ya kwanza tangu nichaguliwe kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba
2015. Hivyo, napenda kuchukua nafasi hii
kuwashukuru Viongozi wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi (TUCTA) na Vyama vyote vya
Wafanyakazi nchini kwa kunialika ili nijumuike nanyi
kwenye Sherehe hizi za Siku ya Wafanyakazi
Duniani mwaka huu. Aidha, napenda kuwashukuru
wafanyakazi wote wa Tanzania kwa kunipa kura
nyingi zilizoniwezesha kuchaguliwa kuwa Rais wa
nchi hii. Naahidi kwenu kuwa sitawaangusha.
Nitumie fursa hii pia kuwapongeza sana wananchi
wa Mkoa Dodoma chini ya Uongozi wa Mkuu wa
Mkoa, Mheshimiwa Jordan Rugimbana kwa
kukubali kuwa wenyeji wa Sherehe hizi pamoja na
maandalizi mazuri mliyofanya kufanikisha sherehe
hizi. Sherehe zimefana, hongereni sana!
Nawashukuru pia wananchi wa Dodoma kwa kunipa
kura nyingi wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka
jana.
Aidha, ninawashukuru sana Wafanyakazi na
Wananchi wote mliojitokeza hapa leo kwa wingi ili
kujiunga na wenzetu duniani kote kusherehekea
siku hii muhimu ya Wafanyakazi Duniani.
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla;
Duniani kote wafanyakazi ni nguzo muhimu ya
maendeleo. Hakuna taifa lolote duniani ambalo
limeweza kuendelea bila kutegemea wafanyakazi
wake. Hapa nchini, wafanyakazi wametoa mchango
mkubwa kwa maendeleo ya taifa letu tangu kipindi
cha ukoloni hadi sasa. Bila shaka wengi wetu hapa
tunafahamu namna wafanyakazi na vyama vya
wafanyakazi vilivyoshiriki kikamilifu katika harakati
za ukombozi wa nchi yetu. Baada ya nchi yetu
kupata uhuru, wafanyakazi wameendelea kutoa
mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu.
Nitumie fursa hii kuwapongeza wafanyakazi kote
nchini kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya kwa
maendeleo ya taifa letu. Ninyi ndio mmejenga
miundombinu mbalimbali tunayoitumia hivi sasa,
ninyi ndio mnahakakikisha Watanzania wanapata
huduma bora za elimu na afya lakini hata ulinzi na
usalama wa taifa letu kwa kiwango kikubwa
unategemea ninyi wafanyakazi. Hongereni sana
wafanyakazi!
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi kwa ujumla;
Kama nilivyotangulia kusema, hii ni sherehe yangu
ya kwanza ya Mei Mosi tangu nimechaguliwa kuwa
Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu. Hivyo,
napenda kutumia fursa hii adimu kuzungumza na
wafanyakazi pamoja na wananchi kwa ujumla
kuhusu masuala na mipango mbalimbali ambayo
Serikali ya Awamu ya Tano ninayoingoza imepanga
kutekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuona nchi
yetu inapata maendeleo kwa manufaa ya
Watanzania wote. Tumejipanga kufanikisha
utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025
pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala.
Sote tunafahamu kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo
inalenga kuiwezesha nchi yetu kuwa ya uchumi wa
kati unaongozwa na viwanda. Ili kutekeleza Dira ya
Maendeleo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala,
tayari tumekamilisha Mpango wa Pili wa Maendeleo
wa Taifa wa Miaka Mitano utakaotekelezwa katika
kipindi cha mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21.
Mpango huu unadhima ya kujenga uchumi wa
viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na
maendeleo ya watu. Lengo kuu la Mpango huu ni
kuhakikisha rasilimali na fursa za nchi zinatumika
vizuri ili kujenga uchumi wa viwanda na kupunguza
umasikini. Baadhi ya malengo mahsusi ni
kuimarisha kasi ya ukuaji mpana wa uchumi kwa
manufaa walio wengi, kuongeza kasi ya kupunguza
umaskini, kuongeza fursa ya ajira kwa wote,
kuongeza upatikanaji na ubora wa huduma za jamii
na kuongeza mauzo nje kwa bidhaa za viwandani.
Ndugu Wafanyakazi na Wananchi;
Baadhi ya masuala muhimu yaliyomo kwenye
Mpango wa Maendeleo ambayo tutayatekeleza
katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja na
kufufua viwanda na kujenga vipya, hususan
vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi
hapa nchini, teknolojia ya kati, nguvu kazi na
ambavyo bidhaa zake zitatumika zaidi hapa nchini,
ikiwemo viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi.
Aidha, tunakusudia mazingira ya uzalishaji na
uendeshaji biashara kwa kuhakikisha tunajenga
miundombinu ya nishati ya umeme, reli, barabara,
maji, madaraja, vivuko, bandari, viwanja vya ndege
na TEHAMA. Tunalenga pia kuhakikisha kuwa
panakuwepo ardhi kwa ajili ya uwekezaji na
upatikanaji wa rasilimali-watu yenye ujuzi.
Halikadhalika, tutaboresha sera, sheria, taratibu,
uratibu na ushirikiano wa kitaasisi.
Maendeleo ya uchumi ni lazima yaende sambamba
na maendeleo ya watu. Ili kuhakikisha hilo,
vipaumbele vitakuwa ni kuhakikisha watu
wanaondokana na umaskini, njaa na ukosefu wa
ajira. Aidha, tutaboresha huduma za jamii, hususan
afya na elimu, kwa kuhakikisha zinapatikana kwa
uhakika na ubora unaostahili. Tutahakikisha watu
wengi wanajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na
pia panakuwepo na usawa wa jinsia na watu wenye
ulemavu, utawala bora, mipango miji na kuogeza
juhudi za kukabiliana na athari za tabianchi.
Matumaini yetu ni kwamba utekelezaji wa Mpango
huu utaleta matokeo chanya kwa nchi yetu kwa
kukuza uchumi kutoka asilimia 7 mwaka 2015 hadi
asilimia 10 mwaka 2020; kuongeza mapato ya
yatokanayo na kodi kutoka asilimia 12.1 ya pato la
taifa mwaka 2014/15 hadi asilimia 17.1 mwaka
2020; kuongezeka kwa kasi ya kupunguza umaskini
ambapo pato la wastani kwa kila mwananchi
litaongezeka kutoka wastani wa dola za Marekani
1,006 mwaka 2015 hadi 1,500 mwaka 2020;
umaskini wa mahitaji ya msingi kupungua kutoka
asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 16.7
mwaka 2020/21; huduma za msingi za afya na
elimu zitaimarika; kuongezeka kwa mauzo nje ya
nchi ya bidhaa za viwandani; kuongeza idadi ya
watalii na kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja
kutoka dola la kimarekani bilioni 2.14 mwaka
2014/15 hadi bilioni 5 mwaka 2021. Hayo ndiyo
malengo yetu.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi
Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa
utagharimu takriban shilingi trilioni 107, zikiwemo
trilioni 59 kutoka Serikalini.Kwa kuanza, kwenye
bajeti ijayo, Serikali imetenga kiasi cha jumla ya
shilingi trilioni 11.82 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo
sawa na asilimia 40 ya bajeti yote kutoka asilimia 26
mwaka uliopita. Kati ya fedha za bajeti ya
maendeleo, shilingi 8.702 trilioni sawa na asilimia 74
ya bajeti ni fedha za ndani na fedha za nje ni shilingi
3.117 trilioni sawa na asilimia 26.
Kama mnavyoona, sehemu kubwa ya ugharamiaji
wa mpango huu itafanyika kwa kutumia fedha za
ndani. Hii ishara tosha kuwa tumedhamiria
kufanikisha azma yetu ya kutekeleza Dira ya Taifa
ya Maendeleo ya mwaka 2025 ili kuleta maendeleo
nchini mwetu na kuwaondolea wananchi kero
mbalimbali.
Ndugu Wafanyakazi na Ndugu Wananchi;
Bila shaka baadhi yenu mtashangaa kwa nini
nimetumia Sherehe hii ya Wafanyakazi kuongelea
malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano katika
kipindi cha miaka mitano ijayo. Jibu ni moja tu.
Imenilazimu kueleza hayo yote ili sisi wafanyakazi
wote hapa nchini tufahamu kazi kubwa iliyopo
mbele yetu. Sisi ndio tunategemewa kuwaongoza
Watanzania katika kutekeleza na kufikia malengo ya
Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Hivyo,
tunaposherehekea sikukuu hii ya wafanyakazi
duniani hatuna budi kila mmoja wetu kujiuliza ni kwa
namna gani tutachangia katika kufanikisha
utekelezaji wa Mpango huu wa Maendeleo kwa nchi
yetu. Kwa kifupi, naweza kusema kuwa mipango
yote mizuri niliyoieleza hapo juu haiwezi kufanikiwa
kama wafanyakazi hawatashiriki kikamilifu.
Hivyo basi, nitoe wito kwa wafanyakazi kote nchi
kila mmoja kwa nafasi yake kujipanga vizuri katika
kutekeleza Mpango huu. Ni lazima tufanye kazi kwa
bidii na kujituma, ueledi mkubwa na uadilifu. Nchi
yetu haitaweza kufikia uchumi wa kati
unaoendeshwa kwa viwanda kama tutaendelea
kulea uvivu, uzembe, ubadhirifu, rushwa, ukwepaji
kodi, kutotimiza wajibu wetu na wafanyakazi hewa.
Kwa kutambua hilo, Serikali yenu imeanza
kuchukua hatua za kuimarisha nidhamu na
uwajibikaji kwa watumishi Serikalini. Tayari
tumeanza kuwashughulikia watumishi wachache
ambao ni wazembe, wavivu, wala rushwa,
wabadhirifu na wasio na maadili.
Nafahamu, watumishi wazembe na wabadhirifu ni
wachache. Lakini watumishi hao ndio wamekuwa
wakiharibu sifa nzuri ya watumishi wa umma. Hawa
ndio wamekuwa wakirudisha nyuma gurudumu la
maendeleo la nchi yetu. Hawa ndio wamekuwa
wakinufaika na kunyonya jasho la wafanyakazi
walio wengi wa Tanzania. Sasa mwisho wao
umefika. Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga
kuwashugulikia popote walipo. Hatutawaonea aibu
au huruma watumishi wa aina hii. Nimefurahi
kusikia Vyama vya Wafanyakazi viko pamoja na
Serikali na havitaunga mkono mtumishi mzembe,
legelege na fisadi. Mmezidi kutupa nguvu zaidi ya
kuendelea na jitihada tulizozianzisha za kurejesha
nidhamu ya kazi kwenye utumishi wa umma.
Niwaombe pia tushirikiane katika kushughulikia
wafanyakazi hewa. Wafanyakazi hewa
wameigharimu Serikali fedha nyingi ambazo
zingeweza kuboresha maslahi ya wafanyakazi
halali na kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo.
Hadi leo idadi ya wafanyakazi hewa waliopatikana
ni 10,295. Kati ya wafanyakazi hao 8,373 ni kutoka
Serikali za Mitaa na 1,922 ni wa Serikali Kuu.
Kutokana na wafanyakazi hao hewa Serikali
imekuwa ikilipa kiasa cha shilingi
11,603,273,799.41 kila mwezi sawa na shilingi
139,239,285,592.92 kwa mwaka sawa na shilingi
696,196,427,964.6 kwa miaka mitano. Fedha hizi
zingeweza kujenga barabara za juu (flyovers) tano
au kuboresha maslahi ya watumishi halali ama
kuboresha huduma mbalimbali za jamii. Aidha,
nafasi hizo hewa zingeweza kutoa ajira kwa
wahitimu wa vyuo vikuu mbalimbali ambao
wanatafuta kazi na hivyo kuleta manufaa kwa taifa.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati nikitoa rai kwa watumishi legelege,
wabadhirifu na wala rushwa kubadilika, napenda pia
kutumia fursa hii kuwapa moyo wafanyakazi wote
ambao ni wachapakazi na ambao wanatekeleza
majukumu yao kwa ueledi na uadilifu. Endeleeni
kufanya kazi kwa kujiamini, kujituma bila ya kuwa
wasiwasi wowote. Nafahamu wapo baadhi ya watu
wamekuwa wakiwatisha na kuwaeleza kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano haijali wafanyakazi.
Wapuuzeni watu hao. Hao ndio wale waliokuwa
wakinufaika au kushirikiana na watumishi mafisadi,
wala rushwa na wabadhirifu. Sasa wanatapatapa
baada ya kuona Serikali inachukua hatua mahsusi
kwa watumishi wa namna hiyo. Serikali ya Awamu
ya Tano haitambuguzi mfanyakazi yeyote ambaye
anajituma na kufanya kazi kwa ueledi na uadilifu.
Nipende kusema tu Serikali yangu itawalinda na
kuwatetea wafanyakazi waadilifu na wachapakazi.
Ndugu Wafanyakazi;
Wakati wa Kampeni na hata nikifungua Bunge
niliwaahidi wafanyakazi wote wa umma na sekta
binafsi kuwa ningeboresha maslahi na mazingira
yenu ya kufanya kazi, ikiwemo kuongeza
mishahara, kuwapatia vitendea kazi, pamoja na
kulinda na haki za msingi za hifadhi ya jamii kama
huduma za afya na malipo ya pensheni baada ya
kustaafu kazi. Ahadi yangu hii bado ipo pale pale na
nawaahidi tena sitawaangusha. Kwa bahati nzuri
hata kaulimbiu ya Mei Mosi mwaka huu ambayo;
“Dhana ya Mabadiliko Ilenge Kuinua Hali ya
Wafanyakazi” inasisitiza umuhimu wa kuboresha
maslahi na mazingira ya kazi ya wafanyakazi.
Kama alivyosema Katibu Mkuu wa TUCTA kuwa
tangu tumeingia madarakani, tumeweza kuongeza
ukusanyaji wa mapato kutokana na kuziba mianya
mingi ya ukwepaji kodi na kudhibiti matumizi yasiyo
ya lazima. Hata hivyo, sio dhamira yetu na bila
shaka sio dhamira ya Watanzania walio wengi
kuona fedha zote tunazokusanya tunazitumia kwa
ajili ya kulipia mishahara watumishi tu. Nasema hivi
ili mfahamu kwamba mapato haya yanawahitaji
wengi sana. Wananchi walio wengi wamepata
matumaini kuwa kutokana na kuongeza kwa
mapato sasa huduma mbalimbali zitapatikana kwa
ubora na uhakika. Hivyo, niwajibu wetu sisi
mliotukabidhi kuongoza Serikali kuhakikisha
tunatumia vizuri rasilimali za nchi kwa manufaa ya
Watanzania wote. Na ninapenda kutumia fursa hii
kuwahakikishia kuwa tutaelekeza fedha
tunazozipata katika maeneo muhimu ambayo
yanamgusa kila Mtanzania, wakiwemo
wafanyakazi.
Ndugu Mwenyekiti wa TUCTA;
Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;
Ndugu Wafanyakazi;
Hivi punde nimetoka kusikia risala yenu nzuri
iliyosomwa na Katibu Mkuu wa TUCTA, Bwana
Nicholas Mgaya. Sitaweza kujibu hoja zote
zilizotajwa kwenye risala yenu. Lakini napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali imezipokea hoja zenu
zote na tutazifanyia kazi. Hata hivyo, naomba
mniruhusu nieleze japo kwa uchache baadhi ya hoja
mliyotaja kwenye risala yenu:
Kwanza, kuhusu suala la kupunguza kodi ya
mapato ya mshahara (PAYE) kwa wafanyakazi.
Napenda kuwaarifu kuwa Serikali yangu kama
nilivyoahidi wakati wa kampeni zangu nimeamua
kuwapunguzia Wafanyakazi kodi ya Mapato ya
Mishahara kutoka asilimia 11 ya sasa hadi asilimia
9 kuanzia mwaka wa fedha wa 2016/17 kutegemea
Wabunge watakavyopitisha bajeti yetu. Tuna
uhakika kwa kufanya hivyo, tutakuwa
tumewapunguzia wafanyakzi mzigo mkubwa wa
makato katika mishahara yao. Nimeamua kuanza
na hili kwanza ili changamoto zilizopo sasa za
kiuchumi tuweze kuzivuka na baadaye mambo
yakiwa mazuri tutaangalia suala la kupandisha
mishahara.
Pili, suala la tofauti ya mishahara. Tayari tumeanza
kuchukua hatua kuhakikisha tunakuwa na mfumo
wa mishahara ambao unazingatia vigezo vya uzito
wa kazi na kupunguza tofauti kubwa ya malipo ya
mshahara kwa kuoanisha mishahara ya watumishi
wa Umma walioajiriwa Serikali Kuu, Serikali za
Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma. Tunataka
Watumishi wa Umma wafaidi matunda ya kazi kwa
kuzingatia uzito wa kazi wanazozifanya kwa misingi
ya haki na usawa.
Aidha, kufuatia marekebisho ya Sheria ya Taasisi
za Kazi Na.7 ya Mwaka 2004, tumeunda Bodi mbili
za mishahara. Bodi ya mshahara katika Sekta
Binafsi inayosimamiwa na Waziri mwenye dhamana
ya masuala ya Kazi na Ajira, na Bodi ya Mshahara
katika Utumishi wa Umma inayosimamiwa na Waziri
mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma.
Majukumu ya Bodi hizi ni kufanya uchunguzi na
kupendekeza kima cha chini cha mshahara katika
sekta husika. Ni matarajio yetu kwamba bodi hizi
zitatekeleza majukumu yake kwa weledi kwa
kupendekeza viwango vinavyozingatia hali halisi ya
uzalishaji, tija na uchumi wetu. Nilikwisha tamka
sitarajii kuwa na mfanyakazi anayelipwa zaidi ya
milioni 15 wakati wengine wanalipwa laki tatu kwa
mwezi.
Tatu, suala la hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya
tano inalenga katika kuhakikisha kwamba wananchi
wengi zaidi watafaidika na mfumo wa hifadhi ya
Jamii nchini kuliko ilivyo sasa. Kwa mfano tunataka
wananchi wengi zaidi wajiunge na Bima ya Afya ili
wawe na uhakika wa matibabu. Tunaendelea na
juhudi ya kupanua wigo wa Mfuko wa Bima ya Afya
vijijini (Community Health Fund) na pia kuwezesha
wafanyakazi wengi wa sekta binafsi kujiunga na
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (National Health
Insurance Fund). Aidha, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii
imeanza kusajili wananchama toka sekta isiyo
rasmi. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba
wananchi wengi wanapata huduma za msingi za
hifadhi ya jamii.
Kwa upande wa kuimarisha Mifuko ya hifadhi ya
jamii pamoja nakuboresha malipo ya Pensheni,
Serikali imekwishaelekeza Mifuko ya Hifadhi ya
jamii kuachana na uwekezaji kwenye miradi
isiyokuwa na tija. Wawekeze kwenye maeneo kama
viwanda ili kuzalisha fursa za ajira na kujipatia
wanachama zaidi. Aidha, ushauri wenu wafanyakazi
kupitia shirikisho lenu la TUCTA kwa Serikali
kuhusu kupunguza idadi ya Mifuko ya Pensheni
nchini na matumizi yasiyo ya lazima umepokelewa
na kukubalika. Lakini ni vyema mfahamu kwamba
kutokana na historia tofauti ya kuanzishwa kwa
mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo sasa, hatua zozote
za marekebisho zinahitaji umakini mkubwa.
Napenda niwahakikishie kwamba kazi ya
kurekebisha mifuko ya Pensheni nchi tutaikamilisha
ndani ya mwaka 2016/2017.
Nne, suala la Vyama vya Wafanyakazi.
Napenda kutoa rai kwa waajiri kote nchini
kutambua kwamba suala hili sio la hiari bali ni
wajibu wao kuwaruhusu wafanyakazi kuanzisha na
kujiunga kwenye vyama vya wafanyakazi sehemu
za kazi bila ya kushurutishwa au kuchaguliwa
chama cha kujiunga. Hivyo, waajiri wote
wanaovunja takwa hili la sheria watachukuliwa
hatua kali. Lakini pia nitoe wito kwenu Viongozi na
wafanyakazi vyama hivyo visitumike kuchocheo
migogoro ya kikazi, uzembe na uvivu kazini na wala
visiwe vyama vya kisiasa kazini. Vyama hivyo
vinapaswa kutumika kuimarisha uhusiano kati ya
waajiri na waajiriwa, kuhamasisha utendaji kazi na
kuleta utulivu sehemu za kazi.
Tano, suala la mikataba ya ajira. Waajiri
wengi wamekuwa hawatekelezi matakwa sheria
kama yalivyobainishwa katika Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 pamoja na
marekebisho yake ambayo tumeyafanya mwaka
2015. Bado yapo malalamiko mengi ya wafanyakazi
kutokuwa na mikataba ya kazi, kufanya kazi bila
vifaa kinga, michango ya pensheni kuchelewa
kuwasilishwa au kutowasilishwa kabisa kwenye
mifuko ya hifadhi ya jamii. Serikali ya Awamu ya
Tano ninayoongoza haitavumilia ukiukwaji huu wa
sheria.
Ili kuhakikisha waajiri wanatekeleza kwa hiari
bila shurti sheria za kazi, tuanza kurekebisha tena
Sheri ya Ajira na mahusiano kazini kwa kuanzisha
adhabu za papo kwa papo ambapo waajiri
watalazimika kulipa faini kwa kila kosa la
kutotekeleza sheria za kazi. Pia, katika mwaka huu
wa fedha, Serikali imetenga fedha kuajiri maofisa
kazi zaidi wapatao 21 ili kuimarisha huduma za
ukaguzi sehemu za kazi. Nitoe wito kwa Vyama vya
wafanyakazi, kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya
Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).
Aidha, ninaziagiza Mamlaka zinazohusika
kusimamia utekelezaji wa Sheria za kazi kusimamia
sheria husika bila woga kwa lengo la kuwalinda
wafanyakazi wasiendelee kutumikishwa na
kunyonywa.
Aidha, naziagiza mamlaka husika
kushughulikia suala la ajira za wageni ambazo
zinaweza kufanywa na wazawa. Hakuna nchi
yoyote duniani ambayo jukumu lake kubwa ni
kuwatafutia ajira wageni kazi ambazo ingeweza
kufanywa na wazawa. Naagiza Wizara zote
zisimamie hili suala kwa nguvu zote ili wazawa
wapate ajira kwanza. Sambamba na hilo, wahusika
wote mshirikiane pia kuwafichua wale wote
watakaofanya kazi bila vibali. Nakumbuka zoezi hili
lilianza sitaki kuamini kuwa ilikuwa ni nguvu za
soda. Mheshimiwa Waziri tafadhali simamia hili.
Suala jingine ambalo nalo limekuwa ni tatizo
sugu ni baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha
michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko ya
hifadhi kwa wakati. Ingawa wafanyakzi wamekuwa
wakikatwa kila mwezi lakini fedha hizo hazifiki
kunakohusika. Tatizo hili pia linaihusu Serikali
kutokana na Hazina kutopeleka michango. Hivyo,
natoa wito kwa waajiri wote nchini kuwasilisha
michango ya wafanyakazi wao kila mwezi bila
kukosa. Hivyo, natoa wito kwa waajiri wote nchini
kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kila
mwezi bila kukosa.
Kwa upande wa Serikali tayari tumeanza
kulishughulikia suala hili la michango kwa kutambua
wafanyakazi wote halali ili michango yao
iwasilishwe. Mathalan, kwenye Mfuko wa PSPF
Serikali ilikuwa ikidaiwa shilingi takriban bilioni 710
bilioni lakini hadi sasa tumelipa takriban shilingi 500.
Ni imani yangu kuwa michango ya inayotakiwa
kulipwa na Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi
itapungua kutokana na zoezi la kuwaondoa
wafanyakazi hewa. Tunaomba Vyama vya
Wafanyakazi vishirikiane na Serikali kufichua
watumishi hewa.
Ndugu Mwenyekiti wa TUCTA;
Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Waheshimiwa Mawaziri na Waheshimiwa Wabunge
mliopo;
Ndugu Katibu Mkuu wa TUCTA;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wafanyakazi;
Mabibi na Mabwana:
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa
kuwashukuru tena Viongozi wa TUCTA na Vyama
vya Wafanyakazi nchini kwa heshima mliyonipa ya
kushiriki kwenye Sherehe hizi. Aidha, napenda
kurudia tena wito wangu kwa Wafanyakazi na
wananchi wote kwa ujumla, tuendelee kufanya kazi
kwa bidii, kwa nguvu zetu zote, kwa maarifa yetu
yote na kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na
uadilifu ili tuweze kusukuma gurudumu la
maendeleo ya nchi yenu. Tuachane na mazoea ya
watu kuingia kazini asubuhi na kuondoka saa nne.
Tukumbuke ya kuwa kazi ni utu, kazi sio
fursa ya kupata mshahara kwa manufaa ya familia
zetu tu bali ni fursa nzuri ya kutoa mchago kwa
taifa lako kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
kijacho.
Mungu Wabariki Wafanyakazi Watanzania!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni kwa Kunisikiliza”.
Source ikilu.go.tz
Jumanne, 24 Mei 2016
Hii ndio hotuba ya mh rais mei mosi 2016
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni